Friday, March 27, 2015

Don Jazzy: Mlinzi aliyefanikiwa kuwa maarufu Afrika



Imeandaliwa na Elizabeth Edward Mwananchi
Posted  Jumapili,Agosti31  2014  saa 11:31 AM

Unapozungumzia watayarishaji wa muziki wanaofanya vizuri kwa sasa barani Afrika lazima jina la Don Jazzy litakuwa kwenye orodha hiyo.
Sifa hiyo inatokana na uwezo wa aina yake alionao mtayarishaji huyu katika kucheza na ala za muziki sambamba na teknolojia, hatua inayomfanya kutengeneza muziki mzuri.
Uwezo huo ndiyo ulimshawishi Kanye West kumuajiri kama mtayarishaji kwenye lebo yake GOOD Music, huo ndiyo ukawa mwanzo wa nyota huyu kutambulika kimataifa.
Akiwa katika lebo hiyo aliweza kutengeneza zaidi ya nyimbo 100 za wanamuziki kadha wa kadha wa kimataifa.

Kama ilivyo kwa watu wengine waliofanikiwa, Don Jazzy hakufikia mafanikio hayo kwa urahisi licha ya kuwa na kipaji cha uimbaji na upigaji ngoma tangu akiwa mdogo.
Kipaji hicho ndicho kilichomsababishia mjomba wake aliyekuwa akiishi mjini London kumualika kwa ajili ya kupiga ngoma kanisani.

Akiwa na umri wa miaka 18 Don Jazzy aliwasili nchini Uingereza na kuanza kupiga ngoma kanisani kazi ambayo pamoja na kumtambulisha haikuweza kumpatia kiasi kikubwa cha fedha.
Hali hiyo ilimsukuma kutafuta shughuli nyingine ya kumuingizia kipato ndipo alipofanikiwa kupata kazi ya ulinzi katika kampuni binafsi.

Muda wote huo Jazzy alikuwa akijifunza kucheza na ala mbalimbali za muziki ikiwamo gitaa la bass kichwani akijiwekea malengo kuwa mtayarishaji siku moja.
Lengo hilo lilitimia miaka michache baadaye aliporudi nyumbani Nigeria akiwa ameweza kwenye utayarishaji na kufanikiwa kufungua studio yake.

Mwaka 2004 aliamua kuunganisha nguvu na rafiki yake wa karibu D’Banj na kuanzisha lebo ya Mo’ Hits Records iliyojizolea umaarufu mkubwa barani Afrika hasa baada ya kurekodi albamu ya No Long Thing.

Wawili hao walidumu pamoja kwa muda wa miaka nane kabla ya Mavin kujitoa na kuanzisha lebo yake ya Mavin Lebo hiyo ilidumu kwa takribani miaka saba kabla ya wawili hao kutengana na Don Jazzy kuanzisha lebo ya Mavin Records huku D’Banj akibaki na Mo’Hits Records.
Akiwa mkurugenzi mkuu wa Mavin Records ameweza kuifikisha lebo hiyo kwenye mafanikio makubwa na kuwa miongoni mwa lebo zinazofanya kazi nzuri kwa sasa nchini Nigeria na Afrika kwa ujumla.
Kwa hivi sasa Don Jazzy ni miongoni mwa watayarishaji ambao wanakimbiliwa na wanamuziki wenye majina makubwa barani Afrika kutokana na namna anavyomudu kutengeneza muziki bora.
Toleo jipya la jarida la Forbes lilimtaja Don Jazzy kama miongoni mwa mastaa wenye nguvu kubwa barani Afrika kwa kushika nafasi ya 36 kati ya magwiji 100.

No comments:

Post a Comment

Ads 468x60px

Featured Posts