Mwaka 2011,
John aliingia Mafinga na kuanza biashara kwa mtaji wa tsh milioni nne na laki
sita(4,600,000/=), na mpaka kufikia sasa biashara yake ina mtaji wa zaidi ya
milioni mia moja.
John aliwezaje kufikia mafanikio haya makubwa?
Hapa John
atatueleza kwa kifupi historia ya maisha yake na kwenye makala nyingine zijazo
atatushirikisha njia alizotumia kuweza kufikia mafanikio hayo makubwa na pia
atatushirikisha changamoto alizokutana nazo na jinsi gani aliweza kuzikabili.
John
anatokea musoma ambapo alizaliwa tarehe 23/03/1988 na kupata elimu ya msingi.
Baada ya kumaliza elimu ya msingi hakuweza kupata nafasi ya kuendelea na elimu
ya sekondari kutokana na hali ngumu ya kifamilia kwa wakati huo. Mwaka 2004
akiwa na miaka 16 John aliamua kwenda Mwanza ambapo hakujua anakwenda kufanya
nini. Alipofika mwanza alifanya kazi ya umachinga kwa miaka mitatu(2004-2006).
Kazi hii ya umachinga ilikuwa ngumu sana kwake na hakuweza kupata fedha za
kutosheleza kujikimu, hivyo aliamua kurudi nyumbani na kwenda kufanya kilimo na
ufugaji.
Akiwa
nyumbani Musoma alipewa taarifa kwamba kuna mtu alikuwa anatafuta mfanyakazi wa
dukani mkoani Mbeya. John alikubali kwenda mbeya kufanya kazi hiyo na tarehe
17/07/2007 alisafiri kwenda mbeya na alipofika alipewa majukumu ya kazi
atakayofanya. Aliambiwa atalipwa mshahara wa tsh elfu arobaini(40,000/=) kwa
mwezi. John alikubali mshahara huu kidogo na kujitoa kufanya kazi ile kwa moyo
mmoja.
Wakati
anafanya kazi hii John alijiwekea malengo ya kuifanya kwa miaka mitano na baada
ya hapo aweze na yeye kuanzisha biashara yake. Kutokana na lengo hili John
alijibana na kuwa na matumizi kidogo sana ya fedha zake ili aweze kuweka akiba itakayomsaidia
kufikia lengo lake.
Mwaka
2011(kabla hata ya miaka mitano kufika) John aliomba kuacha kazi ili aweze
kwenda kuanzisha biashara yake mwenyewe. Wakati huo mshahara wake ulikuwa
umefikia tsh 350,000/=, watu wengi ikiwemo ndugu zake walimshangaa anawezaje
kuacha kazi hiyo inayomlipa vizuri ukizingatia kwamba ana elimu ya msingi tu.
John hakuzingatia hayo kwa sababu alikuwa anajua malengo makubwa aliyojiwekea
na alijua bila ya kuyatekeleza hataweza kupata uhuru aliokuwa anategemea.
Mwaka huo
2011 alifika Mafinga akiwa na fedha taslimu 4,600,000/=. Hakuwa na ndugu yeyote
hapo Mafinga na hivyo alitegemea fedha hii kwenye kuishi pamoja na kuanzisha
biashara. Baada ya kuzunguka na kutafuta alifanikiwa kupata eneo la biashara
ambalo pia ilimlazimu kulifanyia marekebisho hivyo akaanza biashara kwa kununua
mali za duka zenye thamani ya milioni mbili. Biashara aliyoanza na ambayo mpaka
sasa anafanya ni ya kuuza vifaa vya ndani kama tv, magodoro na vifaa vingine
vya kielektroniki.
Mwanzo
biashara ilikuwa ngumu sana na kwa wiki moja ahakuweza kufanya mauzo kabisa.
Hii ilimsukuma kubadili mawazo yake ya ufanyaji wa biashara na kuweka ubunifu
zaidi. Ubunifu alioweka ulimpatia wateja wengi sana ambao mpaka sasa
anauhusiano mzuri na wamemletea wateja wengi zaidi. Ubunifu mkubwa aliofanya ni
kukopesha bidhaa zake kwa makubaliano na pia kujenga urafiki mkubwa na wateja
wake.
Kwa miaka
hii mitatu John ameweza kufikia mafanikio makubwa kwani sasa ana maduka mawili,
duka jingine liko Mkuranga, nje kidogo ya Dar es salaam na ameajiri vijana
sita. Pia ameweza kununua nyumba ya kuishi huko Mafinga, ameweza kununua gari
la biashara na biashara yake kwa sasa ina mtaji wa zaidi ya milioni mia moja.
Kuna mengi
sana utaendelea kujifunza kwa John kwenye makala atakazoendelea kutushirikisha
hapa AMKA MTANZANIA.
Mambo makubwa ambayo nataka
ujifunze kupitia hadithi hii ya John ni haya;
1. John
aliweka malengo makubwa ambayo alifikiri njia za kuyafikia kila siku. Hakuwahi
kujishusha na kuona haiwezekani kufikia malengo yake.
2. John
alikubali kuanzia chini ili kujifunza na kukua. Najua utakuwa umevutiwa na
kutoka milioni 4 mpaka milioni 100 kwa miaka mitatu, ila habari haianzii hapo.
Vitu vilivyomwezesha John kupata mafanikio haya ya sasa ni elimu ya biashara
aliyoipata wakati anafanya umachinga na wakati ameajiriwa.
3. Licha ya
mshahara kidogo, John alipenda kazi aliyokuwa anafanya. Ni muhimu sana kupenda
kile unachofanya, kwa njia hii ndio unaweza kujifunza na kukua zaidi.
4. John
aliweza kuwa na udhubutu wa kuacha kazi ambayo ilionekana kuwa inalipa
kulingana na hali yake na badala yake kwenda kuanza biashara kwenye eneo ambalo
hana uzoefu wala ndugu.
Kuna mambo
mengi sana ambayo kila mtanzania anaweza kujifunza hapa. Na kama mpaka sasa
unalalamika maisha yako ni magumu basi jua umejiamulia mwenyewe. John hakuwa na
vitu ambavyo wewe unalalamika huna. Hakuwa na elimu kubwa, hakuwa na ndugu
aliyempa mtaji wa kuanzia biashara. Alikubali kufanya kazi kwa mshahara kidogo
sana ila akiwa na lengo lake ambalo baadae limefanikiwa.
Ni kipi
kinakuzuia wewe? Elimu? Mtaji? Au hujaamua? Jibu moja naloweza kukupa ambalo
unaweza kulikataa ni kwamba hujaamua. Kwa mambo mengi ambayo umejifunza kwenye
AMKA MTANZANIA kama utaamua kuyatumia sasa utafikia mafanikio makuwa sana.
Makirita Amani amkatanzania.com
ni fundisho zuri kutoka kwa john
ReplyDelete