Tuesday, January 24, 2012

UAMSHO by chrisotpher Mwakasege


UAMSHO
  Je! Ni laana au ni baraka?
(Sehemu ya Kwanza)
Hili swali linakuja kwako – tena kwa wakati wake hasa! Nilikuwa nafundisha katika kanisa fulani hapa nchini – nilipouliza swali hili wengi wakajibu kwa pamoja – ni baraka! Lakini wakati huo huo walikuwako wazee wa kanisa ambao walikuwa wanauona uamsho ya kuwa ni laana!
Nilipokuwa nahubiri kwenye kanisa moja huko Marekani ya kaskazini – Mchungaji na wakristo wa kanisa hilo walinieleza juu ya uamsho uliotokea kanisani hapo miaka michache ya nyuma – na baada ya kipindi si kirefu kanisa likagawanyika na wakristo wengine wakahama, wengine wakarudi nyuma kiroho. Nilipowauliza chanzo cha mgawanyiko huo ni nini – wakajibu bila hata kusita, wakasema “Ni Uamsho!”
  Je! unakubalina na jibu hili ya kwamba uamsho ukitokea katika kanisa huwa unagawa wakristo?
  Sehemu zingine vimetokea vikundi vya uamsho katika makanisa mbalimbali – mahali pengine vimefurahiwa na mahali pengine vimechukiwa, hata kufika hatua hata ya kuvipiga marufuku! Je! hii ni sawa?
  Ni wakati gani uamsho unakuwa ni laana na ni wakati gani uamsho – unakuwa ni baraka? Katika mfululizo huu wa maswali na majibu tutajifunza na kujibu maswali mbalimbali kuhusu Uamsho.
  Ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa mafundisho utakayoyapata katika majibu ya maswali katika mfululizo huu yatakuimarisha zaidi katika maisha yako ya wokovu, na katika kumtumikia Mungu.
  Pia, ni maombi yangu kwa Mungu, katika Jina la Yesu Kristo ya kuwa mafundisho haya juu ya uamsho yatasaidia kutatua matatizo mengi yaliyopo katikati ya Wakristo – hasa yanayotokana na uamsho.
  Ndiyo maana ni vizuri hata wewe uyasome majibu haya ukiwa katika hali ya maombi ili Mungu afungue moyo wako na akili zako upate kuyaelewa na maandiko. Maswali tutakayojibu ni haya yafuatayo:
  SWALI LA KWANZA: Uamsho ni kitu gani?
  Ni rahisi sana kuchanganya maana za maneno na matukio yake, hasa tunapozungumza juu ya Uamsho. Wengine wanachanganya maana ya uinjilisti na ile ya uamsho. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno haya Uinjilisti na Uamsho yana maana zinazotofautiana.
  Neno ‘Uamsho’ limetafsiriwa toka kwenye neno la Kiingereza ‘revival’. Na neno ‘revival’ linatokana na neno ‘revive’ ambalo lina maana ya kuhuisha, kuchochea, kurudishia nguvu, kufufua na kuamsha.
  Kwa mfano Nabii Habakuki alipokuwa anaomba alisema; “ Ee Bwana, FUFUA kazi yako katikati ya miaka …..” (Habakuki 3:2). Na katika Biblia ya Kiingereza ya King James mstari huu umeandikwa hivi; “O Lord, REVIVE thy work in the midst of the years …” kwa maneno mengine Nabii Habakuki alikuwa anaomba juu ya uamsho.
Uamsho unatokea wakati ambapo Mungu, kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu anaposhuka ndani ya mioyo au roho za watu wake ambao wamepoa, au wamerudi nyuma kiroho, au wamekuwa vuguvugu au wamelala. Hawa watu mwanzo walikuwa  wameonja nguvu za Mungu, lakini baada ya muda walirudi nyuma kiroho au wakapoa. Uinjilisti maana yake ni kuitangaza habari njema – au kutangaza habari za Yesu Kristo. Uinjilisti hutumika wakati wa kuwaleta watu wasiookoka katika ufalme wa Mungu. Uinjilisti ni matokeo ya Uamsho katika Kanisa. Kanisa  lililopoa au kulala kiroho huwa halina mzigo wa Uinjilisti wala wa kuleta mavuno ya roho za watu kwenye ufalme wa Mungu.
  Kwa kusisitiza tu ni kwamba Uamsho ni matokeo ya nguvu za Mungu kuwatembelea upya WATU WAKE.
  Nguvu za Mungu zinapowatembelea watu ambao hawajaokoka, na kuwafanya waokoke, hatuliiti tendo hili kuwa ni uamsho, bali ni uinjilisti. Lakini nguvu hizi za Mungu zinapowatembelea watu waliokwisha kuokoka tayari, na kuamsha upya kiu ya kumjua na kumtumikia Mungu, huwa tunaliita tendo hili kuwa ni Uamsho.
  Ndiyo maana ukienda katika madhehebu ambayo kuna wakristo waliookoka na ambao hawajaokoka; wale waliookoka huwa mara nyingi huitwa ‘Wakristo wa uamsho’. Ndiyo maana mara kwa mara unasikia maneno kama haya; mikutano ya uamsho, vijana wa uamsho, watu wa uamsho, maombi ya uamsho, n.k.
  Tunapozungumzia juu ya uamsho, ujue ya kuwa ni lazima kuna kitu cha kuamsha. Kunakuwa na Uamsho, kwa kuwa kuna kitu cha kuamsha. Kunakuwa na ufufuko, kwa kuwa kuna kitu cha kufufuka. Kunakuwa na kuhuisha, kwa kuwa kuna kitu cha kuhuisha.
  Kazi ya kuamsha roho za wakristo waliopoa, au waliorudi nyuma kiroho, au waliolala kiroho, ni kazi ya Mungu mwenyewe, kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu.
  Mtu aliyekuwa ameokoka akirudi nyuma na kufa kiroho, kazi ya kumfufua au kumwamsha upya si ya mwanadamu bali ya Roho Mtakatifu.
  Ingawa ni kweli kwamba Mungu humshirikisha mtu amtakaye katika kazi zake mbalimbali kama tutakavyoona kadri tunavyoendelea; bado mwanzilishi na msimamishaji wa uamsho ndani ya mtu ni Mungu mwenyewe.
  Si vyema kumpa mwanadamu sifa ya kuleta uamsho mahali fulani, badala ya kumpa Mungu ambaye amemtumia mtu huyo kama chombo tu.
  Fahamu “si kwa uwezo (wa mwanadamu), wala si kwa nguvu (za mwanadamu), bali ni kwa ROHO YANGU, ASEMA BWANA WA MAJESHI” (Zakaria 4:6)
SWALI LA PILI: Kwa nini Mungu analeta Uamsho?
  Ukisoma katika Biblia utaona ya kuwa kuna sababu mbili kubwa ambazo zinamfanya Mungu alete uamsho katikati ya watu wake.
  Sababu ya Kwanza ni UAMSHO WA KAZI YA BWANA. Nabii Habakuki aliomba hivi, “Ee Bwana, FUFUA KAZI YAKO katikati ya miaka; katikati ya miaka tangaza habari yake; katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2).
  Sababu ya Pili ni UAMSHO WA MIOYO YA WATU WA MUNGU. Mtunga Zaburi aliomba hivi; “Je, hutaki kurudi na KUTUHUISHA (Kutuamsha), watu wako WAKUFURAHIE? (Zaburi 85:6). Na katika kitabu cha Nabii Isaya 57:15 imeandikwa hivi; “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu na kuifufua mioyo yao waliotubu”.

1.  Uamsho wa kazi ya Bwana

  “Ee Bwana, FUFUA KAZI YAKO katikati ya miaka; katikati ya  miaka tangaza habari yake; katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2)
  Nilipoyasoma maombi haya ya Nabii Habakuki nilijiuliza maswali kadhaa, na baadhi yake ni haya: Je! kazi ya Bwana maana yake nini? Je! kazi ya Bwana nayo inahitaji kufufuliwa? Kitu gani kinaua kazi ya Bwana hata ihitaji kufufuliwa?
  Maswali haya yalinifanya nianze kukisoma kitabu cha Nabii Habakuki kwa makini. Nilipokuwa nakisoma, niliyakuta mambo ambayo ningependa kukushirikisha hapa.
  Kitabu cha Habakuki kwa sehemu kubwa kinaeleza mazungumzo kati ya Mungu na nabii wake Habakuki. Habakuki anaanza kwa manung’uniko na malalamiko juu ya uharibifu wa haki, na kutokuonekana kwa kazi au uwepo wa Mungu katikati yao.
  “ Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia    kwa sababu ya UDHALIMU, ila hutaki KUOKOA. Mbona wanionyesha uovu, na unitazamisha UKAIDI? Maana UHARIBIFU NA UDHALIMU u mbele yangu; kuna UGOMVI, na MASHINDANO yatokea. Kwa sababu hiyo SHERIA INALEGEA, wala HUKUMU HAIPATIKANI;  kwa    maana watu wabaya huwazunguka wenye haki, kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka” (Habakuki 1:2-4).
  Ni wazi kwamba katikati ya wana wa Israeli – uzao wa Ibrahimu, kulitokea UDHALIMU, UKAIDI, UHARIBIFU, UGOMVI, MASHINDANO, UVUNJAJI WA SHERIA, na HAKI  KUTOKUWEPO. Habakuki hakuona ya kwamba ni halali kwa mambo hayo kuwepo katikati ya watu wa Mungu, na Mungu wao akae kimya.
  Na Mungu alimjibu kuwa atalitumia kabila la Wakaldayo kuwaadhibu wana wa Israeli (Habakuki 1:5 – 11)
  Katika mahojiano yake na Mungu, Habakuki anakubali kabisa ya kuwa wana wa Israeli wamekosa. Lakini anamwuliza Mungu ya kuwa kwa nini Yeye, aliye mtakatifu, tena mwenye macho safi asiweze kuuona uovu huo (Habakuki 1:12 – 13), na kwamba amewachagua Wakaldayo wapagani, ili watwae kisasi juu ya taifa teule.
  Nabii Habakuki alitaka kujua kwa nini Mungu ameamua kuwaadhibu wana wa Israeli kwa uovu wao kwa kuwatumia Wakaldayo walio waovu zaidi kuliko wao. Tena, kwa nini amsaidie Mkaldayo aliye mjeuri asiye na haki, ili apate ushindi? Kwa maneno mengine alitaka kufahamu kwa nini ujeuri, ugomvi na dhuluma vitawale mataifa na si haki na amani?
  Mungu alimpa Nabii wake Habakuki majibu mawili muhimu; 1. Mwishoni haki itashinda;
2. “Mwenye haki ataishi kwa imani yake” (Habakuki 2:4).
  Baada ya mazungumzo hayo, ndipo Nabii Habakuki alipoomba sala hii “ Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka, katikati ya miaka tangaza habari zake, katika ghadhabu kumbuka rehema” (Habakuki 3:2)
  Kwa maneno mengine alikuwa anamwomba Mungu kuwa badala ya kuadhibu akumbuke rehema ili awarehemu watu wake. Utendaji wa kazi yake ufufuke au uamke kwa upya katikati ya watu wake. Palipo na ugomvi alete amani. Palipo na dhuluma alete haki. Palipo na mashindano alete ushirikiano. Palipo na ukaidi alete upole na unyenyekevu.  
Je! huoni kuwa na sisi tunahitaji kuungana na Nabii Habakuki kuomba juu ya uamsho wa kazi ya Mungu katika makanisa na vikundi vya watu wa Mungu kama vya maombi vilivyopoa? Katikati ya Wakristo kazi ya Mungu haionekani. Kumejaa dhuluma, ukaidi, ugomvi na mashindano.
  Wakati umefika wa wewe na mimi kumwomba Mungu kwa juhudi ili kazi yake na matendo yake yaonekane tena katikati yetu. Palipo na ugomvi atuletee amani ipitayo fahamu zote. Palipo na mashindano atuletee ushirikiano katika Roho na kweli. Palipo na dhuluma atuletee haki na hukumu za kweli zisizokuwa na upendeleo. Palipo na ukaidi atuletee upole na kunyenyekea. Palipo na kuuchukia wokovu, alete kuupenda wokovu. Palipo na uchovu na uzito wa kuifanya kazi ya Mungu, alete utayari na wepesi badala yake! Kama ulikuwa hujaanza kuomba, basi anza sasa kwa ajili ya mahali unapotaka mabadiliko yatokee kwa wakristo wote kwa ujumla. Pia umwombe Mungu kuwa “katika ghadhabu akumbuke rehema”.
  2.   Uamsho wa mioyo ya watu wa Mungu
“Je! hutaki kurudi na KUTUHUISHA, Watu  wako  AKUFURAHIE?" Zaburi 85:6)
  Tafsiri nyingine ya maneno haya inasema hivi:
“Je hutatujalia tena maisha mapya ili watu wako wakufurahie?”
  Na katika maneno ambayo Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake yanayozungumza juu ya FURAHA MIOYONI MWAO – alisema hivi;
  “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea   kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. FURAHINI    NA KUSHANGILIA; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa   mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 5:11,12).
  Ukiona mtu aliyeokoka anakosa amani na furaha wakati anaposhutumiwa, anapoudhiwa, na anaposingiziwa uongo kwa sababu ya KUMWAMINI YESU, ajue ya kuwa amepoa kiroho na anahitaji uamsho. Yesu alisema yanapotokea hayo FURAHI na KUSHANGILIA.
  Pia, Yesu Kristo alisema hivi:
  “  Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa FURAHA. Mwanamke azaapo yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya FURAHA YA KUZALIWA MTU ULIMWENGUNI. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na MIOYO YENU ITAFURAHI, na FURAHA YENU hakuna awaondoleaye. Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin, nawaambia, mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata furaha yenu iwe timilifu  " (Yohana 16:20 – 24).  
Furaha ya Bwana ndani ya mioyo yetu sisi tulio wakristo, ndiyo nguvu ya kutuwezesha kuendelea katika wokovu bila manung’uniko. Ukiona mtu anasema ameokoka na huku amekosa FURAHA YA BWANA ndani yake, basi ujue kuna shida fulani katika maisha yake ya kiroho!
  Katika kitabu cha matendo ya Mitume furaha inaonekana wazi katikati ya wakristo hawa wa kwanza. Furaha inaonekana walipopokea nguvu za Roho Mtakatifu (Matendo ya Mitume 13:52). Furaha inaonekana Bwana alipofanya miujiza katikati yao (Matendo ya Mitume 13:8). Furaha inaonekana katikati yao walipoona watu wengine wakiokoka na kumfuata Yesu (Matendo ya Mitume 15:3). Na pia furaha inaonekana walipokuwa wakiumega mkate (Matendo ya Mitume 2:46).
  Na mtume Paulo katika nyaraka zake kwa waumini anazungumzia furaha katika maeneo mawili muhimu. Kwanza, anazungumzia juu ya furaha aliyonayo anapowaona wale aliowaongoza kwa Yesu wakiendelea katika imani ya wokovu (1Wathesalonike 2:19; Wafilipi 2:2). Pili, anazungumzia furaha anayopata yeye na mkristo yoyote yule anapoteswa kwa ajili ya Kristo, kwa kuwa si furaha ya kibinadamu, bali ni furaha iliyo tunda la Roho ndani ya mtu (Wagalatia 5:22).  
Ni wazi kabisa ya kuwa Mkristo asipoonekana ana FURAHA YA BWANA, basi hata maisha yake ya kiroho yanakosa changamoto. Na wengine hufikia hata kuacha wokovu.
Nakumbuka wakati fulani mtu mmoja alinifuata kwa ajili ya ushauri na akasema hivi; “Mimi nimeokoka, lakini naona napata mawazo ya kutaka kuacha wokovu, na niliona kabla ya kufikia uamuzi huo nije kwako unishauri”
Mara moja nilifahamu ya kuwa amekosa FURAHA katika njia hii ya wokovu. Baada ya kuzungumza na kumweleza kitu cha kufanya kufuatana na maandiko, nilimwambia asiache wokovu. Nikamuuliza “Ukimwacha Yesu utakwenda kwa nani? Namshukuru Mungu ya kuwa huyo mtu alipokea ushauri niliompa na anaendelea na wokovu.
  SWALI LA TATU: Uamsho ukitokea mahali kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu, mambo gani yanatokea?
  Uamsho unapotokea katikati ya watu wa Mungu, kuna mambo mengi yanayotokea, lakini mambo makubwa yafuatayo hujitokeza:
  1.  Hofu ya Mungu
Palipo na uamsho pana hofu ya Mungu. Kuna wakati unafika ambapo watu wa Mungu wanapoa na kutokujali sana mambo ya Mungu, na kutokupenda maombi ya muda mrefu, na hata kufikia kutokwenda kanisani au kwenye vipindi vya masomo ya biblia, kwa kujisingizia shughuli nyingi.
  Ukiona mambo haya yanajitokeza au yamejitokeza, basi ujue ya kuwa hofu ya Mungu haipo kati yao.
  Na Mungu anapoamua kujidhihirisha upya katikati yao kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, kunatokea uamsho, na uwepo wa Mungu unakuwa wazi kwa kila mtu. Na palipo na uwepo wa Mungu, pana hofu ya Mungu.
  Hofu ya Mungu inapotokea katikati ya watu wa Mungu inaleta mambo mpya. Ikiwa umekaa na watu waliookoka utakuwa umeona ya kuwa, hofu ya Mungu isipokuwepo katikati yao, huwa wengi wao wanaenenda bila ushuhuda na bila hekima, na matokeo yake ni kuleta makwazo na kuufanya Wokovu udharauliwe.
  Lakini hofu ya Mungu inaporudi katikati yao kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu, wanaanza upya kutembea katika ushuhuda na hekima. Je, unafahamu ni kwa nini? Kwa kuwa imeandikwa; “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, ……” (Zaburi 111:10).
  Tafsiri nyingine ya hofu ya Mungu ni kumcha Bwana. Mungu anapojidhihirisha upya katikati ya watu wake, kila mmoja wao anaona kama vile Mungu ameshuka kwa ajili yake tu na ameshuka kumshughulikia yeye tu! Kwa hiyo utaona watu wakiwa wepesi kutubu dhambi zao na kutengeneza maisha yao ya kiroho.
  Na kinachofuata ni watu hao kuanza kujishughulisha upya na mambo ya Mungu. Utaona wanapenda utakatifu, utaona wanapenda maombi na kumtumikia Mungu. Kunapotokea uamsho watu huona Mungu yuko karibu nao zaidi kuliko alivyokuwa zamani.
  Nakumbuka nilikuwa nahubiri mahali fulani hapa nchini, na niliposema wale wanaotaka kutubu waje mbele, watu wengi walikuja na kutubu kwa machozi, Roho wa Mungu alishuka kwa nguvu katika mkutano ule.
  Na nilipowafuatilia hao waliotubu, nikaona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni watu waliokuwa wameokoka zamani lakini wakarudi nyuma na kuanguka dhambini. Na neno lilipohubiriwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, wakachomwa mioyo yao, wakawa kama watu walioamshwa toka usingizini, wakaamua kutubu na kumrudia Bwana.
  Na matokeo yake ni vikundi vya maombi kuanza kwa upya; ‘Fellowship’ na kanisa kupata nguvu mpya, na watu kushuhudia kwa ujasiri na bila woga. Hii si kazi ya mtu, ni kazi ya Roho Mtakatifu aichunguzaye mioyo ya watu na kuijua ilivyo.
  2.   Watu wengi wanaokoka
  Watu wa Mungu wakipoa, hata watu wanaozaliwa upya mara ya pili wanakuwa wachache. Watu wa Mungu wakiamka upya kiroho, watu wengi wanaokoka. Ni wazi kwamba kunapotokea uamsho, mavuno ya roho za watu yanakuwa mengi – kwa kuwa watu wanapata msukomo mpya wa kushuhudia.
  Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo.
  Siku ya Pentekoste ilipotimia. Roho wa Uamsho aliwashukia wale wanafunzi wa kwanza wa Kristo, ambao walikuwa wamejaa hofu na wasiwasi; na baada ya kuwaamsha na kuwavika ujasiri walianza kumsifu Mungu kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.  
Uamsho huu katikati ya wanafunzi wa Kristo, ulileta mafadhaiko na mshangao kwa wale ambao hawakuwa wanafunzi wa Kristo. Imeandikwa: “Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa …. Wakashangaa wote ….” (Matendo ya Mitume 2:6,7).
  Na wakati ule ule Petro ambaye alikuwa amewahi kumkana Yesu Kristo mara tatu Roho Mtakatifu alimpa ujasiri wa kusimama na kuhubiri kwa nguvu habari za Yesu Kristo.
Mtu aliyeamshwa na Roho Mtakatifu akisema maneno yake huwa yamejaa moto ambao huwachoma wale ambao wanamsikiliza!
  “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo Yao, wakamwambia Petro na Mitume wengine, Tutendeje ndugu zetu? Petro akawaambia, tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina la Yesu   Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashu hudia Kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake (walioamua kuokoka) wakabatizwa na    siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu”  (Matendo ya Mitume 2:37 – 41).
  Kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu katikati ya watu wa Kristo, watu wengine ELFU TATU waliokoka kwa siku moja na kwa mahubiri ya mtu mmoja, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu!
  Na hawa waliookoka si kwamba walitubu na kutawanyika bali biblia inasema, “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu …… Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa” (Matendo ya Mitume 2:42 – 47).
3.  Uamsho unaleta Umoja
  Watu wa Mungu wakipoa kiroho, matengano, magomvi na mashindano hutokea katikati yao. Watu wa Mungu wakipoa kiroho, huwa wanapambana wao kwa wao badala ya kupambana na shetani.
  Watu wa Mungu wakipoa kiroho hata baraka za Mungu hazionekani katika makusanyiko yao, ndoa zao, na kazi zao. Wanakuwa ni watu wanaoishi kwa kujitahidi, na siyo kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
  Imeandikwa hivi:
“Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana (Wagalatia 5:25 – 26)
“Tazama jinsi ilivyo vema, na kupendeza ndugu wakae pamoja,   kwa  UMOJA.………….. maana ndiko Bwana ALIPOAMURU BARAKA, Naam uzima hata milele” (Zaburi 133:1-3).
  Hii ni habari njema kusikia ya kwamba BWANA AMEAMURU BARAKA ZAKE ZIENDE KWA WATU WANAOKAA PAMOJA NA KWA UMOJA!
  Ni kweli kwamba vitu vingi vinaweza kutukusanya pamoja, kama vile ndoa, harusi, misiba, mikutano, ibada, ugomvi, mashauri; nakadhalika. Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mnao umoja.  
Narudia tena: Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mnao umoja. Mnaweza kuwa pamoja katika ibada au harusi huku moyoni hampatani. Na hivi ndivyo ilivyo kwa watu wengi wa Kristo, wanakaa au wanakutana pamoja lakini hawana Umoja!
  Umoja wa kweli hauletwi na taratibu za kibinadamu hata kama ni nzuri sana. Zinaweza kutufanya tuwe pamoja, lakini haziwezi kutufanya tuwe na umoja. Umoja wa kweli huletwa na Roho Mtakatifu.
  Ndiyo maana Roho Mtakatifu akijidhihirisha kwa upya katikati ya watu wa Mungu huwa wanapatana na kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti ya madhehebu yao! Mipaka ya mapokeo ya kidhehebu, ya kikabila, ya kiutajiri, ya kimaskini, huwa inavunjika!
  Ndiyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Kristo wa kwanza walipohuishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Ukisoma katika kitabu cha Mtendo ya Mitume 2:41 – 42 utaona jinsi wenzetu walivyoishi kwa Umoja.
  Imeandikwa:  “Nao waliolipokea Neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika USHIRIKA, na katika kuumega mkate, na katika KUSALI ……. Na wote  walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu  vyote SHIRIKA wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa MOYO MMOJA walidumu katika   hekalu, wakimega mkate NYUMBA KWA NYUMBA na kushiriki chakula chao kwa FURAHA na kwa MOYO MWEUPE, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa   WAKIOKOLEWA”.
  Kunapotokea uamsho, umoja wa kweli hutokea. Kulipo na uamsho wa Roho Mtakatifu, ushirikiano wa kweli hutokea. Kunapotokea uamsho, uchoyo unahama, ugomvi unahama, wivu unahama, uvivu unahama, na ubinafsi unahama. Na tabia ya uamsho ni kuleta umoja wa kweli – watu waliopoa kiroho wanaamka toka katika uchoyo, toka katika ugomvi, toka katika ubinafsi na wivu, na badala yake wanaanza kushirikiana, kusaidiana, kupendana na kusali pamoja katika Roho Mtakatifu.  
Wakristo wenzentu wa mwanzo ndivyo ilivyotokea kwao Roho Mtakatifu alipotawala maisha yao na uhusiano wao – tunasoma hivi:
“Na jamii ya watu waliamini (waliookoka) walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali WALIKUWA NA VITU VYOTE SHIRIKA. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu miongoni mwao mwenye MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile walivyouza, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadri ya alivyohitaji”  (Matendo ya Mitume 4:32 – 35)
  Hata hivi leo maisha ya namna hii yanatokea na ushirikiano wa namna hii unatokea ikiwa Roho Mtakatifu ataruhusiwa kuleta uamsho kwa utaratibu wa Mungu wenye kuleta baraka na siyo utaratibu wa kibinadamu au wa kishetani unaoleta laana

36 comments:

  1. Amina hapa ni kwa neema ya bwana

    ReplyDelete
  2. Nimeelewa mtumishi. Barikiwa sana

    ReplyDelete
  3. hili somo ni zuri sana , kwa viongozi wa makanisa na makundi mbalimbali ,kama tunahitaji mabadiliko tusome tena na tena.

    asante mwalimu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amina na hakika

      Delete
    2. Amen, Amen!! Nimebarikiwa Sana na somo na Kuna kitu kimeongezeka ndani yangu! Mungu akubariki Sana baba

      Delete
    3. Nmebarikiwa mno

      Delete
    4. Nmebarikiwa mno

      Delete
    5. Amen, nimebarikiwa sana. Nimepata marifa

      Delete
  4. UAMSHO AGENDA YETU Nguvu Zaidi tunamtaka bwana na nguvu zake barikiwa sana mwalimu

    ReplyDelete
  5. Amen nimebarikiwa

    ReplyDelete
  6. Amen nimeelewa na nitalifanyia kazi kwa jina la Yesu

    ReplyDelete
  7. Barikiwaaaaaaaaaa Sana Mwalim

    ReplyDelete
  8. Thank you mtumishi nimekuelewa na nimekubali na nimejifunza pia Mungu alie hai atusaidie

    ReplyDelete
  9. Nimelewa.zaidi ya nifikirivyo ! Neno uamsho!/barikiwa sana Mwalimu wa neno LA Mungu.

    ReplyDelete
  10. Nimeelewa sana ๐Ÿ‘

    ReplyDelete
  11. Mungu amenifundisha kupitia mafundisho haya mwalimu Mungu akupe neema ya kufika mbali.

    ReplyDelete
  12. Mungu abariki na kuingilia kati kwenye vikundi na viongoz walioko makanisa tu ๐Ÿ™๐Ÿ™๐Ÿ™๐Ÿ™

    ReplyDelete
  13. Nimekuelewa sana mtumishi wa Mungu ubarikiwe sana.

    ReplyDelete
  14. Mungu aishie aendelee kukutumia zaidi sikuyajua haya

    ReplyDelete
  15. Kila nikisoma hii huwa napata nguvu mpya,Mungu akubariki sana mtumishi wa Mungu

    ReplyDelete
  16. Mungu akubariki mwl kwa SoMo zuri na Mungu anipe kuliishi

    ReplyDelete
  17. asante mumishi wa MUNGU kwa mafundisho hayon mazuri.

    ReplyDelete
  18. Nashukuru mno kukutana na hekima ya mwl. Hakika nimejifunza vitu vingi Katika somo hili. Barikiwa mno baba

    ReplyDelete
  19. Mungu akubariki Sana mtumishi wamungu kwasomo zuri nimeelewa sana

    ReplyDelete
  20. Amina nimebarikiwa saana nami nitafundisha somo hili kanisani

    ReplyDelete
  21. Ameen ubarikiwe mtumishi wa Bwana๐Ÿ™

    ReplyDelete
  22. Ameen ๐Ÿ™ nimetoka na kitu kipya leo

    ReplyDelete

Ads 468x60px

Featured Posts